Katika eneo la milima, kusini mwa Tanzania, kuna kijiji kimoja ambacho kinaitwa Wangama. Katika kijiji hicho, watu wa kabila la Wabena huishi. Wanazungumza Kiswahili na Kibena. Wanakijiji wenye bidii hukuza vyakula vingi vizuri kama vile viazi, mahindi, vitunguu, nyanya, na kadhalika.
Hata hivyo, maisha ya watu katika kijiji hicho si rahisi kila wakati. Kiko mbali na miji mikubwa, kwa hivyo mambo muhimu kama vile huduma za afya, shule, na utunzaji wa mazingira yanaweza kuwa magumu. Wananchi wanakabiliwa na safari ndefu na za gharama kubwa kwenda kwenye vituo vya afya, na wakati mwingine, hawapati huduma bora za matibabu. Shule zilizopo zinakabiliwa na upungufu wa walimu na vifaa vya kufundishia, hivyo kusababisha elimu duni kwa watoto. Pia, suala la utunzaji wa mazingira lina changamoto, kwani uharibifu wa ardhi na uchafuzi wa mazingira unaweza kuathiri maisha ya wanakijiji kwa muda mrefu.
Hata hivyo, katika mwaka wa 2017, matumaini yalianza kung'aa kwa wanakijiji wa Wangama. Watu wawili wenye mioyo wa ukarimu na kujitolea, waliamua kuchukua hatua na kuanzisha shirika linaloitwa Wangama Foundation. Waliona haja ya kuleta mabadiliko chanya katika kijiji hicho, na hivyo wakaamua kuchukua hatua ya kuanzisha shirika ambalo lingeweza kusaidia kuleta huduma bora za afya, elimu, na kutunza mazingira. Kuanzishwa kwa Wangama Foundation kulikuwa mwanzo wa safari ya matumaini na ustawi kwa wanakijiji.
Shirika hilo lilijenga kliniki ambayo husaidia watu walio na virusi vya ukimwi na kuwapa na matumaini. Kliniki hii sasa inahudumia wagonjwa kwa upendo na huduma bora za matibabu, ikitoa dawa muhimu na ushauri kwa wale wanaohitaji. Zaidi ya hayo, Wangama Foundation imeanzisha programu za elimu na ufadhili wa masomo kwa watoto walio na uhitaji, ikilenga kuwapa fursa sawa za elimu na kuwawezesha kufikia ndoto zao. Jambo hili limeleta faraja kwa familia zenye changamoto za kifedha, ambazo sasa zimepata matumaini katika elimu ya watoto wao.
Shirika hilo pia limeanzisha miradi ya kijamii inayolenga kutunza mazingira ya eneo hilo. Miradi hii inatia ndani upandaji wa miti, usafi wa mazingira, na kampeni za kuelimisha watu kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.
Kupitia juhudi hizi za wafadhili na wanakijiji, Wangama Foundation imeleta mabadiliko mazuri ambayo yanazidi kuimarisha ustawi na maendeleo ya kijiji cha Wangama.
No comments:
Post a Comment